Yesu ni Mwanzilishi wa Pumziko la Milele?

KARIBUNI TENA KATIKA KULITAFAKARI NENO LA MUNGU WETU ALIYE HAI

“INAWEZEKANA KUISHI MILELE”

EDDIEe

SOMO LA NNE LINASEMA: Yesu ni Mwanzilishi wa Pumziko la Milele?
Dr. Edward MhinaFungu Kuu: “Na uzima wa milele ndio huu wa kujue wewe, MUNGU wa pekee wa kweli, na YESU Kristo uliye mtuma” Yohana 17:3

Downloadable Version: Yesu Ni Mwanzilishi Wa Pumziko La Milele?

Na. Dkt. Edward Raphael Mhina

Biblia inafundisha kuhusu habari za pumziko la milele. Siku ya Sabato. Sabato ni pumziko ambalo MUNGU alimpatia mwanadamu kama zawadi siku ya saba ya uumbaji. Ukisoma katika kitabu cha Mwanzo kinazungumzia uumbaji ambao MUNGU aliufanya kwa kutamka ‘Neno’, na katika kitabu cha Yohana 1:1-3 anazungumzia huyo ‘Neno’ ni YESU Kristo. Hii huthibitisha ya kwamba YESU aliiumba Sabato. Tunaona pia katika bustani ya Edeni MUNGU anawapa Sabato wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa.

Pumziko hilo ni la milele zote, hadi mbingu mpya nan chi mpya zitakazofanywa na Mungu mahali ambapo watu watakaookolewa wataishi mbele za Mungu milele, watakatifu wa Mungu wataendelea kupumzika katika siku hii, Isaya 66:22-23, “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.”

Katika mafundisho ambayo watu wamesoma maanadiko na kuyaelewa vibaya ni pamoja na hili la Sabato ndio maana leo utakuta kuna makanisa/madhehebu mengi ya wanaoabudu siku tofauti tofauti za juma lakini tujiulize katika vichwa vyetu je, ni siku gani ambayo MUNGU wetu alikusudia tuitunze ikiwa kama zawadi yake kwetu?. Ukisoma katika kitabu cha Kutoka 20:8-11 “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa..”

Utashangaa jinsi Mungu alivyo wa upendo maana hii ni amri/kanuni ya nne katika zile kanuni/ amri kumi ambazo MUNGU alitupatia ili tuishi milele. Lakini kanuni hii imeanza na neno ikumbuke ikiwa na maana ya kwamba MUNGU alikwisha itoa hapo mwanzo alipoiumba dunia na kuwapa wazazi wetu wa kwanza , hivyo anatukumbusha kuitunza kama alivyo kusudia.

jesus and the sabbathNdugu msomaji nisipo lisema hili ambalo moyo wangu unanisukuma kukuambia nita ulizwa na MUNGU kwanini sikuliandika. Ukweli ni kwamba watu wanajaribu kupindisha ukweli juu ya siku hii ya saba ya kila juma ambayo ni Sabato lakini napendekeza kwako kuiangalia biblia pekee kama mwongozo wa maisha yetu kwamba inatuambia nini. Wengi husema ya kwamba Sabato ilikoma pale msalabani lakini YESU mwenyewe anasema kupitia Mathayo 5:17-18
“Msidhani ya kwamba nilikuja kuitangua torati au manabii,la, sikuja kutangua ,bali kutimiliza,18 Kwa maana amini nawaambia ,mpaka mbingu na nchi zitakapo ondoka ,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka , hata yote yatimie” Hakuna kilicho futwa katika amri za MUNGU ikiwemo sabato ndani yake.

Wote tunaamini ya kwamba YESU alifufuka siku ya tatu kutoka kaburini na wengi huamini ya kwamba Ijumaa kuu ni siku ambayo YESU alikufa alishinda kaburi Jumamosi na na siku ya tatu yani Jumapili akafufuka ambayo wengi husheherekea. Siku hiyo ya Jumapili katika maandiko matakatifu inaonesha ya kwamba ni siku ya kwanza ya juma soma nami katika Mathayo 28:1 “Hata sabato ilipo kwisha, ikapambazuka siku ya kwanza ya juma. Mariamu Magdalena na Mariam yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi” hivyo tunaweza kusema ya kwamba hata YESU alitunza Sabato kwa kutofufuka siku ya saba ya juma ambayo ni Jumamosi. Ukweli ni kwamba lazima tufuate kile kinachoelezwa katika biblia na kama sisi kweli ni wakristo ikiwa na maana ya kwamba tuna mfuata kristo yeye anasema hivi katika Marko 2:28 “Basi mwanawa Adamu ndiye BWANA wa sabato” hivyo twapaswa kufuata kile ambacho yeye anataka tufuate. Napendekeza kwako kuishika sabato ya MUNGU katika biblia na si ile iliyowekwa na mwanadamu hizo Sabato za kimapokeo ambayo watu wengi kwa kuifuata huku wakiijua Sabato ya kweli kama ilivyofunuliwa katika maandiko matakatifu watakosa uzima wa milele.
Sali nami sala hii ninapohitimasha somo hili:

MUNGU muumbaji wa Sabato nisaidie niuelewe ujumbe huu na kwa haraka nifanye matengenezo, kuwa mwalimu wangu ninapoendelea kujifunza masomo haya, kwa njia ya Roho wako Mtakatifu uwe kiongozi wangu pekee, ukinithibitisha imani yangu na kunituliza katika kweli ya Neno lako, na unisaidie nisikose somo linalofuata. Kwa jina la YESU KRISTO amen!
KARIBU TENA TUTAENDELEA KUTAFAKARI NENO LA MUNGU KATIKA SEMINA HII.

SOMO LA LINALOFUATA: Kuishi Maisha ya Milele

Maswali, Maoni au Ushauri wasiliana nami: +255652648737 au +255768678122

Advertisements

“UTUSAMEHE MAKOSA YETU”

Ev. Peter JeftahNa Ev. Peter Jefta

Simu; +255 757 916 891

Barua pepe; jefterpeter@yahoo.com

Mathayo 6:12utusamehe deni zetu kama sisi nasi tuwasemehevyo wadeni wetu”

Downloadable version: Utusamehe Makosa Yesu

Yesu akiwa mlimani akiwafundisha wanafunzi wake pamoja na makutano wote ilimlazimu kuwafundisha hata namna ya kusali maana huenda aligundua miongoni mwao walikuemo wasiojua kusali sawasawa, lakini pia miongoni mwao walikuemo watu waliosali kwa namna ya tofauti isivyopasa.

Tazama huenda wengine walisali kama huyu; Luka 18:10-12 “lakini Yule farisayo akasimama akiomba hivi………… na kwasababu ya sala za namna hii ilimlazimu Yesu kutoa fundisho la namna ya kusali. Dhumuni lingine pia la Yesu kuwafundisha hawa wapendwa namna ya kusali ni kuwaepusha katika sala za wamataifa za kupayuka; Mathayo 6:7,”nanyi mkiwa katika kusali msipayuke payuke kama watu wa mataifa maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.

Na kwa sababu hiyo yesu anatoa kielelezo cha namna tunavyopaswa kusali Mathayo 6:9-13 9basi ninyi salini hivi Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje,10, mapenzi yako yatimizwe,hapa duniani kama huko mbinguni. 11, utupe leo riziki yetu. 12utusamehe deni zetu kama nasi tuwasemehevyo wadeni wetu. 13 na usitutie majaribuni lakini Christ - Sermon on the Mount 1 - Harry Andersonutuokoe na Yule mwovu [kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu, hata milele Amina].

Mada yetu ya leo inajengwa katika fungu la 12, (utusamehe deni zetu kama nasi tuwasemehevyo wadeni wetu) katika namna iwavyo vyote kila tuombapo ni LAZIMA tukiri na kuungama dhambi zetu mbele za MUNGU kwa sababu wanadamu tu wadhambi na mioyo yetu imejaa dhambi tupu Mwanzo 6:5Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analoliwaza moyoni mwake ni baya tu siku zote”. Na hivyo basi yatupasa kila mara tufanyapo maombi tusalimishe nia zetu kwake yeye aliye juu zaidi yetu.

Lakini tazama neno hili lina mtihani ndani yake ambalo tunapaswa kulijibu… utusamehe kama nasi tusamehevyo. Kwanza kabisa imetupasa kusameheana sisi kwa sisi kabla ya kuomba msamaha kwa MUNGU ndipo sala hiyo itapokuwa imekamilika. Lakini leo imekuwa ni maajabu au tuseme imekuwa ni kawaida sana kwetu wanadamu kuomba msamaha kwa MUNGU wakati sisi kwa sisi tumetofautiana katika mawazo, maneno, au kwa namna tofauti tofauti.

Tena haishangazi kwa kumkuta mtu kanisani au mahala popote pa ibada akiomba tena akidhani anaomba kwa dhati sana akimsii MUNGU amsamehe makosa yake maana kakumbuka dhambi za huko nyuma lakini pia wakati mwingine akiomba kwa msisitizo mkubwa juu ya mbaraka kwake na kwa jamaa yake lakini hafikirii juu ya yule ndugu aliyemkosea au yule aliekataa kumsamehe kwa sababu tu ya kuwa ameshamsamehe mara nhyingi sana au mpaka mkosaji atimize kusudi fulani.

Mpendwa habari ni hii tukisameheana sisi kwa sisi ndipo BWANA atatusamehe Mathayo 6:14, “kwa maana mkiwasemehe watu makosa yao na Baba wa mbinguni atawasemehe”. Lakini habari mbaya ni hii Mathayo 6:15bali msipowasehe watu makosa yao wala Baba yenu hatawasemehe ninyi makosa yenu.

Na kwa sababu hiyo imetupasa hata sasa kabla ya kuomba tena kwanza tuwafikirie wale waliotukosea na tuwasemehe tena bure kabisa bila kigezo wala gharama yoyote

Na kama endapo kuna mtu umemkosea imekupasa kupatana nae kwanza ndipo uombe toba halisi kwa MUNGU maana hiyo ndiyo ibada ya kweli. Marko 11:25, 26. “25 Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. 26 Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

jesus provides forgivenessLakini je imetupasa kusamehe mara ngapi maana huenda mwingine rafiki yako jamaa yako au ndugu yako amekuchosha kwa makosa ya kila mara tena kwa kujirudia rudia, Mathayo 18:21,22; kasha petro akamwendea akamwambia Bwana ndugu yangu anikose mara ngapi name nimsahe? Sikiliza jibu la Yesu katika fungu la 22, Yesu akamwambia sikuambii hata mara saba bali hata saba mara sabini.

Kwa akili ya kibinadamu tumekuwa tukifanya hesabu ya namba hii na kuleta jibu la kwamba huenda ikawa ni mara 490, lakini swali ni je akikukosea mara ya 491 utamfanyaje? Lengo la Yesu hapa haikuwa ni kutuambia idadi ya kiasi tunachopaswa kusamehe bali tuelewe yakwamba kusamehe ni wajibu wetu hata kama itajirudia mara nyingi kiasi gani.

Huenda kuna namna fulani unashindwa kupatana na ndugu au rafiki uliyekosana nae, labda njia ya kupatana nae imekuwa shida au huenda ugumu upo kwake hayupo tayari kupatana nawe ipo suluhidho katika hili mpendwa Mathayo 18:15-17;” na ndugu yako akikukosa enenda ukamwonye…………………………” kwa uongozi wa Roho mtakatifu kwa ombi la dhati ukimuombea pia adui yako hakika MUNGU atafungua njia ya upatanisho leo hii.

Fikiria ni nani labda ni ndugu jamaa au rafiki yako mmetofautiana kwa muda sasa ipo kazi mbele yako ya kufanya upatanisho upya ili na MUNGU wako wa mbinguni akusamehe. Fikiria kupatana na adui yako leo ili sala yako ikubalike nawe uhesabiwe haki mbele za MUNGU usiendelee kufanya ibada bandia huku umeshajua ibada halisi ni ipi.

MUNGU akubariki unapopanga kufanya hivyo. Kama ndiyo nia yako na MUNGU akusaidie kutimiza sasa katika jina la YESU AMINA!

Somo hili limeandaliwa na

EV. PETER I. JEFTER

Phone; 0757 916891

Email; jefterpeter@yahoo.com

Wasiliana nasi kwa maswali, maoni na ushauri kuhusu somo hili.

UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI KAMA MRADI

Ev. Mujaya Mujaya

Ev. Mujaya Mujaya

Na. Ev. Mujaya Mujaya

Simu: +255715678122 au +255768678122

Barua Pepe: ev.mujaya@gmail.com

Downloadable Version:Ufugaji Wa Kuku Wa Kienyeji Kama Mradi

MAHITAJI

 1. Kuku(tetea) 10 na Jogoo 01
 2. Banda bora
 3. Vyombo vya chakula na maji
 4. Chakula bora
 5. Madawa na chanjo kwajili ya magonjwa
 6. Chanzo cha nishati joto na mwanga
 7. Elimu na ujuzi wa malezi bora
 8. Chombo au chumba cha kutunzia vifaranga
 9. Mayai ya kuku wa kisasa/mayai mabovu(ambayo hayakuanguliwa)
 10. Madaftari au kitabu cha kutunzia kumbukumbu

KUKU 10

Wakati wa kuanza mradi wako hakikisha una kuku 10 (matetea) wenye umri sawa na hawajawai kutaga hata mara moja. Chagua kuku wenye rangi nzuri kutoka katika familia bora kutegemea malengo ya mradi wako. Mfano kama lengo lako ni kuzalisha kuku wa kienyeji kwajili ya nyama basi chagua mbegu ambayo inakuwa haraka na yenye uzito mkubwa. Au ikiwa lengo ni mayai basi ni vema kuchagua aina ya kuku yenye kukua haraka na kutaga mayai mengi.

Ili kupunguza gharama za manunuzi ya kuku na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji ni vema kununua kuku wadogo ambao wametoka tu kuachishwa kulelewa na mama zao. Kuku hawa utawapata kwa bei ya chini, tena watafaa sana maana watakua na umri mmoja pia.

JOGOO 01

Jogoo mmoja tu anatosha kuwahudumia kuku matetea yote kumi. Hakikisha katika uchaguzi wa jogoo bora lililochangamka, rangi mzuri, upanga umesimama, macho angavu, uzito wa kutosha, rangi nzuri na uwezo mkubwa wa kuzalisha. Ni vema mfugaji akaelewa kwamba kuku wote watakaozalishwa watategemea ubora wa jogoo wake. Uwezo wa kutaga kwa kuku na upatikanaji wa mayai pia hutegemea kwa karibu ubora wa jogoo aliyechaguliwa.

BANDA BORA

Miongoni mwa mambo mhimu naya kwanza kuzingatiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kama mradi ni maandalizi ya banda bora. Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Mfugaji anatakiwa kuandaa banda lenye ukubwa wa mita 10 kwa mita 04. Yani urefu uwe mita 10 na upana upana wa mita 04. Kisha kata vyumba vya mita 2 urefu na upana mita 4 kutoka katika banda lako hivyo utakuwa na jumla ya vyumba vitano vyenye ukubwa unaolingana. Ujenzi uzingatie malighafi na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira husika. Mfano katika maeneo ambayo fitoKuku zinapatikana kwa urahisi banda linaweza kuandaliwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo. Au sehemu ambayo mabanzi hupatikana kwa urahisi basi banda laweza kujengwa kwa kutumia mabanzi. Vifaa vya kujengea banda vizingatie pia gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-

 • Sakafu: Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
 • Kuta: Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
 • Paa: Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
 • Wigo: Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati

Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

 • Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.
 • Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
 • Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
 • Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala.
 • Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga.
 • Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji.
 • Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa. Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga.

JINSI YA KUFANYA

Wakuze kuku wako hadi watakapofikia muda wa kutaga. Wakianza kutetea ni kiashiria kwamba wakati wa kutaga umekaribia hivyo andaa viota kwajili ya kutagia.

Viota vinapaswa viwe na ukubwa stahiki ili kumwezesha kuku kuyafunika mayai yote vizuri wakati wa kuetamia, viota viwe vinavyozuia mayai kutawanyika, viwe mahali pakavu na safi.

Hakikisha kuku wote wanataga katika viota tofauti. Kuku anapotaga IMG_20140306_153739mayai matatu unapashwa kuchukua mayai mawili na kumwachia yai moja ili kumfanya aendelee kutaga zaidi. Kuku akifikia yai la kumi na mbili anza kumwachia mayai matatu ili kumwandaa kwa kazi ya kuetamia. Kwa kufanya hivi, kuku atataga mayai 15 au zaidi na ikiwa atataga mayai 15 au chini ya hapo nakushauri utafute mayai mengine ujazilizie ili kufikisha mayai 20 kwa kila kuku. Zingatia kwamba mayai unayoyatoa kwa kila kuku, yanatunzwa sehemu salama, mahali pakavu, pasafi na penye joto la wastani.

Kuku wote wanapaswa kuanza kuetamia kwa siku moja. Ili kufanikisha hili inapasa uwe karibu na kuku wako. Kuku mmoja akianza kuetamia mwekee mayai ya kuku wa kisasa au mayai mabovu ya kuku wa kienyeji. Utafanya hivi hadi kuku wako wote watakapoanza kuetamia mayai. Kuweka mayai mabovu au mayai ya kuku yaliyotumika humfanya kuku aendelee kuetamia akijua ni mayai yake.

Baada ya kuona kwamba kuku wako wote wapo tayari kwa kuetamia mayai, waandalie banda maalumu kwajili ya kuetamia yani chumba kimoja katika lile banda letu. Ninashauri kwamba chumba kwajili ya kuetamia kiwe chumba cha kwanza au cha mwisho katika mfuatano wa vyumba vya banda lako. Andaa viota bora vya kuetamia, weka mayai 20 kwa kila kiota, ikiwa hayajatimia unaweza kununua kwa wafugaji wengine ili kuifikia idadi yako.

Waamishe kuku kutoka wanapotagia na kuwaweka katika chumba ulichokiandaa kwajili ya kuetamia. Ili ufanikiwe katika zoezi hili inafaa lifanyike wakati wa usiku na unafanya katika giza. Mweke kuku katika kila kiota na asubuhi wajikute kila mmoja katika kiota chake. Wahudumie kwa chakula na maji ya kutosha. Wakati wa usiku waongezee joto la ziada kwa kuweka jiko au ndoo ya chuma yenye chengachenga za mkaa au kama una umeme weka taa za joto.

Baada ya siku 21-25 kuku wako wataanza kuangua vifaranga. Huu ndio wakati unaotakiwa kuwa karibu sana na kuku wako kuliko wakati wote. Watenge vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa; waweke katika chumba chao maalumu mbali na kuku. Kama chumba cha kuetamia kilikuwa cha kwanza basi vifaranga wawe chumba cha mwisho n.k

Ukishawatenga vifaranga mbali na matetea wako, wawekee tena mayai mengine 20 kila tetea, mayai ambayo utayanunua kwa wafigaji wenzako. Hakikisha kuku waliotaga hayo mayai ni wazuri, hawana magonjwa na wanauzito/ukubwa unaofaa. Mayai yote yakaguliwe vizuri ili kujua kwamba yameharibika, yana nyufa au mabovu. Kabla ya kuweka mayai mengine hakikisha chumba chako ni kisafi na viota vimesafishwa, havina wadudu na uchafu wowote. Kuku wako bila kujijua wataanza kuetamia upya mayai uliowawekea.

Ukiwawekea mayai rudia mzunguko kama nilivyokwambia awali. Baada ya siku 21 hadi 25 tena utapata vifaranga wako wengine tena. Fuata kila hatua kama nilivyokwambia hapo awali. Lakini kwa awamu hii nashauri waache matetea wako wapumzike wala usiwapatie mayai mengine tena.

JINSI YA KULEA VIFARANGA

Ikikaribia siku ya 20 tangu ulipowawekea matetea wako mayai katika chumba cha kuetamia, andaa chumba kwa ajili ya kulea vifaranga. Safisha kwa kuondoa uchafu na wadudu wote.

Washa taa ya joto au weka chombo cha kutoa joto katika chumba cha vifaranga nusu saa kabla hujaIMG_20141114_104757anza kuingiza vifaranga wako. Weka pia chakula na maji ya kutosha katika vyombo vyenye umbile na ukubwa utakaowawezesha vifaranga kuvitumia. Tandaza magazeti, maboksi, makaratasi n.k katika sakafu ya chumba hicho. Hakikisha vifaranga wako hawajikusanyi sehemu moja maana wakifanya hivyo wengi wao watakufa ili ufanikiwe katika jambo hili, banda lako liwe la mduara katika kona zake.

Weka joto la kutosha. Joto la kutosha ni lile linalowafanya vifaranga watawanyike chini ya chanzo cha joto wakati kama joto limezidi vifaranya kukimbia mbali na chanzo cha joto na ikiwa joto halitoshi vifaranga hujukusanya chini ya chanzo cha joto.

Baada ya siku 3 utawapatia chanjo ya Gumboro na siku 7 wapatie chanjo ya New Castle, utarudia tena kuwapa chanjo hii baada ya mwezi mmoja kisha utafanya hivi kila baada ya miezi mitatu mitatu.

MAPATO YA MRADI WAKO

Katika uzazi wa kwanza utapata vifaranga 150 kwa wastani wa vifaranga 15 kwa kila kuku. Tuseme haujazingatia kanuni za ufugaji za makala hii ukapata vifaranga 100 yani wastani wa vifaranga 10 kwa kila kuku. Kisha baadaye wakakua wakafa kuku 50 yani watano kwa kila kuku utakuwa na jumla ya kuku 50.

Baada ya wiki 3 utapata tena kuku tufanye kwa mahesabu kama hayo hapo juu kwa hasara utakuwa na kuku wengine 50, na kufanya jumla ya kuku 100. Ikiwa kuku wako baada ya uzao wa pili uliwapumzisha kwa miezi miwili basi mwezi wa 3 utapata tena kuku vifaranga 100 na wiki 3 baadaye utapata wengine 100. Kwa mahesabu kama hayo awali wakikuwa utakuwa na kuku wengine 100 ambao watakuwa.

Baada ya miezi 6 utakuwa na kuku wakubwa wa uzao wa kwanza 50, uzao wa pili kuku 50 na utakuwa na kuku wenye umri wa miezi mitatu 50 wa uzao wa 3 na kuku wengine 50 wa uzao wa 4.

Katika kuku 100 wa uzao wa kwanza na pili, tufanye kuku 50 wawe matetea ukijumlisha na kuku 10 ulioanza nao mradi utakuwa na matetea 60. Ikiwa kila tetea atatotoa vifaranga 10 na vikakua vitano tu, mwishoni utakuwa na kuku 300 na baada ya miezi mitatu kuku wengine 900 toka katika kutoka kwa uzao wa kwanza, wapili na watatu. Hivyo mwaka wa pili utafunga na kuku si chini ya 1,200/= wanaotaga mayai.

Ukiuza majogoo yote 1,200/= kwa bei ya 8,000/= ili upate pesa ya kujenga miundombinu bora maana sasa utakuwa na kuku wengi wanaoendelea kuzaliana kwa kasi utapata pesa kiasi cha TZS 7,200,000/=. Sasa ongeza kuku wako wa kutaga hadi wafikie kuku 4,000 maana sasa utakuwa na pesa za kutosha kuendesha mradi wako.

IMG_20140309_101614Sasa ukiwa na kuku 4000 wa kienyeji wa kutaga mayai, ikiwa kuku 3000 tu watataga ukauza yai moja kwa bei ya haraka haraka ya TZS 250 tu, utapata TZS 750,000/= kwa siku ambayo sawa na TZS 22,500,000/= kwa mwezi na TZS 270,000,000/= kwa mwaka sawa sawa na 128,572 USD. Kumbuka mwamba makadilio haya niya chini sana. Ukifata kanuni zote kwa makini na maombi huku ukimtanguliza Mungu utafikia hata TZS 500,000,000/= kwa mwaka.

Kumbuka unapofanikiwa kupata mapato ya kila aina, umtolee Mungu zaka(x10%) ya mapato yako, pia ukatoe sadaka ambayo ni kubwa kuliko zaka na uwasaidie masikini na wahitaji.

Tunza kumbukumbu zako zote za fedha katika daftari maalumu kuhusu mapato na matumizi ya mradi wako. Pia hali ya kuku wako kuhusu tarehe za chanjo ya mwisho, siku walipoanza kuetamia, magonjwa yanayowasumbua mara kwa mara n.k

Wasiliana nasi kwa maswali, maoni au ushauri.

NAMNA YA KUFANYA UCHAGUZI

Ev. Mujaya Mujaya

Ev. Mujaya Mujaya

Na. Ndg. Mujaya Mujaya

Simu: +255715678122 na +255768678122

Barua pepe:   ev.mujaya@gmail.com

Downloadable Version:Namna Ya Kufanya Uchaguzi

Njozi, kuweka vipaumbele vya maisha na njia bora za kufanya uchaguzi ni mambo muhimu sana kujifunza katika maisha yetu. Mambo haya matatu yanatufanya tuwe jinsi tulivyo sasa na jinsi tutakavyokuwa siku za usoni. Kupata au kukosa ufalme wa mbinguni hutegemea sana Njozi, Vipaumbele na Chaguzi tunazozifanya.

Katika maisha tunalazimika kufanya uchaguzi kila siku na kila wakati. Tunachagua tule nini, tuvae nini, tukae wapi, tujenge nyumba gani na wapi, tununue gari au tujenge nyumba? Hivyo jinsi tulivyo ni jumla ya chaguzi tunazozifanya kila siku na tunazoendelea kuzifanya. Na endapo tutachagua kutochagua tutakua tumechagua kutochagua.

Uchaguzi mwema huwa na matokeo mema wakati uchaguzi mbaya huwa na matokeo mbaya pia. Pia chaguzi njema hujenga mwisho mwema na kwa upande mwingine chaguzi mbaya hujenga mwisho mbaya. Lakini hata uchaguzi wetu ungeleta matokeo mabaya na ya kuumiza kuasi gani, wengi tunapofanya uchaguzi tunakuwa na matarajio mema kwa kiasi fulani. Tunakuwa kwa ujinga, kutojali au kupuuzia tunapumbazwa na mazingira yanayotuzunguka na kupelekea ufanywaji wa maamuzi/chaguzi mbaya. Kwa mfano Lutu alipewa uhuru na Ibrahimu kuchagua eneo la milki aitakayo akachagua eneo aliloliona linapendeza kwa macho yake kama bustani ya Mungu, lakini mwisho wa uchaguzi wake ulikuwa kukosa kila kitu. Mwanzo 13:8-13

“Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma. Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya Bwana.”

Kuna changamoto kubwa zinazotupata sasa ambazo zinatokana na chaguzi zetu tulizozifanya kipindi fulani kilichopita. Changamoto ambazo zingezuilika au zisingekuwepo kama tungefanya chaguzi sahihi. Pia kuna mafanikio tuliyonayo leo ambayo yanatokana na chaguzi ambazo tumezifanya siku zilizopita, mafanikio ambayo tusingekuwa tumeyapata kama tusingechagua vema.

Hatari kubwa tuliyonayo kama vijana ni kufanya uchaguzi mbaya maana kila mara tufanyapo uchaguzi mvuto wetu upo katika upande mbaya na hivyo vijana wengi wanajikuta katika matokeo mabaya bila kujua kwa chaguzi mbaya walizozifanya katika maisha yao siku zilizopita. Katika mambo ambayo Mungu ametuachia uhuru sisi kama viumbe wake ni uchauchaguziguzi. Tunaweza kuchagua kumpendeza au kumhuzunisha. Mbele yetu Mungu ameweka uzima na mauti, Baraka na laana lakini kazi ya kuchagua ameiacha katika mikono yetu. Kumbukumbu la Torati 30:19

“Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;”

Katika aya hii tunapata ukweli mwingine kwamba, tunafanya uchaguzi baada ya kubarikiwa na Mungu. Tunafanyia uchaguzi zawadi na baraka za Mungu maishani mwetu. Baada ya kubarikiwa, ndipo tunachagua mwenendo au mwelekeo wa maisha yetu. Yoshua 24:15

“Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana”

Kuna baadhi ya chaguzi ambazo tunaweza kurekebisha matokeo yake lakini kuna chaguzi nyingine ambazo hatuwezi kurekebisha matokeo yake yawe mema au mabaya. Kwamfano uchaguzi wa mwenzi wa maisha katu hatuwezi kubadilisha uchaguzi wetu tunapokuwa tumekwisha kuufanya na kuingia katika ndoa. Katika chaguzi ambazo hatuwezi kutawala au kubadilisha matokeo yake ni vema sana kumuomba Mungu sana kabla ya kufanya uchaguzi. Kwa mfano Danieli aliomba mara tatu kwa siku alipochagua kumwabudu Mungu wa mbinguni badala ya Mfalme Dario. Danieli 6:10

“Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.”

GHARAMA YA UCHAGUZI

Kila uchaguzi unaofanyika una gharama yake. Gharama hii ni fursa unazoamua kuzipoteza kwa kufanya au kutofanya uchaguzi wako. Gharama ya uchaguzi haikwepeki kwakuwa tuna njia chache sana za kutimiza mamilioni ya mahitaji yetu. Kwa mfano:-

 1. Umepata TZS 10,000,000/= na unahitaji kufanya uchaguzi au kutofanya uchaguzi wa mambo yafuatayo kuitumia au kuiweka benki tu. Ikiwa utaitumia unaweza kwa fedha hiyo kufanya mambo yafuatayo kama kununua kiwanja au shamba, kununua gari, kufungua biashara mpya, kuanzisha kilimo au ufugaji, kulipa ada yako ya masomo, kutoa huduma kwa jamii, kusaidia ujenzi wa kanisa. Sasa ikiwa utatumia pesa kununua kiwanja inamaanisha kwamba umepata gharama/hasara ya mambo mengine yote ambayo haujayachagua yani kwa uchaguzi wako wa kiwanja umekubali kukosa gari, biashara mpya, kilimo au ufugaji, ada ya masomo, huduma yako kwa jamii au Yesu.
 1. Umefikia wakati wa kuona au kuolewa na una wasichana/wanawake zaidi ya 100,000 nchi nzima lakini unatakiwa umchague mmoja tu. Kumchagua mmoja ambaye mchafu, hajui kupika, mpuuziaji wa mambo ya kiroho, amayeharibu mali ya familia na kanisa, mgomvi, asiyeheshimu watu wa nyumbani kwake, mbishi n.k humaanisha umekubali kuingia gharama/hasara ya kumpoteza mke ambaye ni msafi, anayejua kupika, anayemheshimu Mungu, mtunzaji wa mali ya Mungu na familia, mpole, mwenye heshima, mpatanishi, mcheshi n.k na kwa mume kadhalika.
 1. Unahisi kiu na unahitaji kutosheleza kiu yako. Katika jambo hili unaweza ukachagua mambo mengi sana, kwa mfano maji safi na salama au maji yasiyochemshwa, maji yaliyosindikwa au maji ambayo hajayasindikwa, je, kwa sharubati au soda, je soda ya aina gani? Coka, Fanta, Tangawizi, Sprite n.k? je, maziwa au bia? Na uchaguzi wa njia moja humaanisha umepoteza njia nyingine zote na manufaa yake kwa kutimiza kiu yako.

Wakati mwingine hatuwezi kuchagua maana tunajikuta tu katika matokeo tuliyochaguliwa. Hakuna hata mmoja wetu aliyechagua wazazi au familia ambayo angezaliwa, rangi ya ngozi yake, urefu au ufupi n.k

JINSI YA KUFANYA UCHAGUZI SAHIHI

Uchaguzi tunaoufanya unategemea sana uzoefu wetu wa maisha, muda, njia za kutatua mahitaji yetu na mazingira yanayotuzunguka. Uchaguzi sahihi ni ule wenye matokeo mazuri na gharama/hasara ndogo kwa kuchagua au kutochagua. Njia za kufanya uchaguzi hutofautiana baina ya mtu na mtu kwa sababu ya uzoefu tofauti, njia/fursa za kutatimiza mahitaji, muda na mazingira yanayozunguka.

Hapa ni baadhi ya kanuni au njia za jumla ambazo unatakiwa kuzitumia sehemu yoyote unapokuwa katika kufanya uchaguzi wowote ule. Njia hizo ni kama zifuatazo:-

 1. Mwombe Mungu.

Katika kuomba tunamwambia Mungu mahitaji yetu wazi wazi ili atuongoze katika uchaguzi mwema. Kuna chaguzi njema ambazo twaweza kufanya ikiwa tutaomba ambazo hatuwezi kuzipata ikiwa hatutaomba. Mfano: Daudi alimuuliza Mungu kwa maombi kila wakati kabla ya kufanya uamuzi au uchaguzi, 1 Nyakati 14:9-11

“Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai. Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako. Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, Bwana amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.”

Maombi yanaonesha kwamba tunamtumaini Mungu kama mwezeshaji na mpaji wa mahitaji yetu pia ndiye kiongozi pekee kuelekea uchaguzi sahihi. Mithali 3:5IMG_20141213_153615

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

Katika swala la uchaguzi wa mwenzi wa maisha, neno la Mungu linasema:-

kama wanaume na wanawake wana mazoea ya kuomba mara mbili kwa siku kabla hawajafikia kuoa au kuolewa, basi wangepaswa kuomba mara nne kwa siku wakati hatua kama hiyo inatarajiwa kuchukuliwaAH 71

Wakati mwingine tunapoomba tunajiinua na kutaka mapenzi yetu yatimizwe na Mungu kama tutakavyo sisi na hivyo kumshusha Mungu kuwa kama si kitu. Hii ndiyo sababu ambayo tunashindwa kuchagua vizuri kwa sababu ya ubinafsi wetu katika maombi. Yakobo 4:3

“Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”

Kinyume cha kuomba vibaya kwa ubinafsi na kumshurutisha Mungu afuate mwenendo wa tama zetu, neno la Mungu linatushauri kwamba sala na mtazamo wetu wakati wa maombi uwe kama ifuatavyo:-

“Sala yako na iwe hii, ‘Nitwae, Ee Bwana, niwe wako kamili…’ Mkabidhi yeye mipango yako yote, itekelezwe au kuachwa kama maongozi ya Mungu yatakavyokuonesha.” SC 70

Mtazamo wako uwe ni huu Yeremia 42:6,

“Likiwa jema au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya Bwana Mungu wetu,… ipate kuwa faida yetu tunapotii sauti ya Bwana, Mungu wetu.”

 1. Soma maandiko matakatifu

Katika kusoma maandiko matakatifu (Biblia na roho ya unabii) tunaweza tukajua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu kwamba Mungu anataka tufanye nini. Katika kusoma maandiko tutaona jinsi watu wacha Mungu walivyofanya chaguzi zao au walishughulikiaje changamoto zao na hivyo kutupatia msingi wa kufanya chaguzi zetu.

Katika maandiko tutaona jinsi ambavyo Mungu ametoa ahadi mbalimbali ambazo kwa kuzidai kwa maombi na imani Mungu atatupatia.

Visa vya mashujaa katika maandiko vitatutia moyo nasi tuenende katika chaguzi au njia zao ili tufikie miisho mizuri kama wao wakati visa vya watu waliofanya chaguzi mbaya vitatukemea tusifuate njia zao maana tutaangamia.

 1. Weka vipaumbele

Kwa sababu kuna njia chache sana za kutimiza mahitaji yetu mengi sana hivyo tunatakiwa kuweka vipaumbele vya maisha kwamba nini kianze na tumalizie wapi. Lile jambo la kwanza linafaa kuwa linalotimiza mahitaji mengi sasa na baadaye kwa gharama ndogo sana ya kuchagua au kutochagua.

Tatizo lipo katika kuweka vipaumbele, yani jambo la mwisho linakuwa la kwanza na jambo la kwanza linakuwa la mwisho. Katika vipaumbele kuna mambo ambayo yanategemeana kwa mfano ili kijana aanzishe familia yake kuna baadhi ya maandalizi anayotakiwa kuyafanya hivyo basi kama kipaumbele chake kitakuwa kuanzisha mji basi kabla ya kuoa atatakiwa kutimiza maandalizi yote.

Katika vipaumbele vyetu vyote Mungu. Mapenzi na ufalme wake ndiyo yapasa kuwa kipaumbele cha kwanza. Maana yake ni kwamba kabla haujaweka kipaumbele cha kwanza juhoji kwamba je, Mungu amekubali niendelee katika njia hii? Jambo ambalo Mungu ameliruhusu kutendeka litafanyika kwa ufanisi na utoshelevu mkubwa. Mathayo 6:31-33

“Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Katika mahitaji yako yote kunabaadhi ya mahitaji ambayo kwa kuyapata hayo utakuwa umetimiza sehemu kubwa ya mahitaji mengine. Katika kuweka vipaumbele, anza na mahitaji haya ambayo kwa kuyatimiza utakuwa umefanya sehemu kubwa ya mahitaji yako kwa gharama ndogo ya uchaguzi.

 1. Fanya uchambuzi wa kina na kuhesabu gharama

Kabla ya kufanya uchaguzi lazima ufanye uchambuzi wa kina wa vipaumbele vyako ili kuhesabu gharama au hasara zinazoweka kutokana na uchaguzi wako. Katika kufanya uchambuzi wako jihoji je, kwa kufanya hivi nitapata nini? Je, kwa kufanya hivi nitakosa nini? Je, kwa kutofanya hivi nitapata nini? Je, kwa kutofanya hivi nitakosa nini? Baada ya uchambuzi huo chagua njia ambayo itakuwa na sababu njema nyingi za kufanya kuliko kutofanya lakini kwa hasara/gharama ndogo za uchaguzi au mambo utakayoyakosa kwa kufanya uchaguzi.

 1. Waone watu wazoefu wacha Mungu

Inafaa sana wakati wa mtanziko kuhusu uchaguzi wa kufanya, kupata ushauri kwa watu wenye uzoefu. Watu hao wanapaswa kuwa wacha Mungu maana kutoka kwao unaweza kupata mwongozo wa mapenzi ya Mungu kutokea katika uzoefu wao wa imani.

Mithali 11:14 “Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”

Mithali 15:22 “Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.”

Hatari kubwa inayotukabili vijana ni kujiona ya kwamba tunahekima kubwa kiasi cha kutosha kuwa washauri wetu wenyewe. Neno la Mungu linatwambia kwamba:-

“Lakini wengi miongoni mwa vijana wamechagua kuwa washauri na viongozi wao wenyewe, na mambo yao wameyachukua mikononi mwao wenyewe” MYP 444

“Kama wewe umebarikiwa kuwa na wazazi wacha Mungu, basi omba ushauri wao. Weka wazi mbele yao matumaini na mipango yako, jifunze mafunzo yako kutokana nan a kile walichojifunza katika maisha yao, nawe utasalimika usipate maumivu mengi ya kichwa. Juu ya hayo yote, mfanye Kristo kuwa mshauri wako, Jifunze neno lake kwa maombi.” MH SAM_1035359

 1. Kiasi

Kiasi ni kutotenda kabisa mambo maovu na kutenda kwa busara/hekima mambo mema. Shetani anazunguka zunguka ili kutupotosha tumchague yeye au tuchague vibaya ili tupate maafa lakini Mungu anasema kwamba ili kumpinga twapaswa kuwa watu wa kukesha katika sala, imani na KIASI.

1 Petro 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

1 Wathesalonike 5:6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

1 Petro 1:13 Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

2 Timotheo 4:5 Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.

1 Wathesalonike 5:6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

1 Wathesalonike 5:8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

Vifupisho:

AH_Adventist Home

MYP_Messages to Young People

SC_Steps to Christ

Wasiliana nasi kwa maswali, maoni na ushauri.