MUNGU ATAPONYA UPOFU WETU

Na. Ev Mujaya M.J

Fungu Kuu: Luka 4:18

Upofu umeghubika maisha yetu ya kila siku watu hawajui wafanye nini kutatua changamoto zinazowakabili; hawajui nini hatma ya maisha yao siku za usoni. Upofu huu upo katika nyanja mbalimbali za maisha kiuchumi, kijamii, kiutamaduni za zaidi sana kiroho. Matokeo ya upofu yamekuwa ni maisha duni, malalamiko na manung’uniko, msongo wa mawazo n.k

1. Upofu wa Bartimayo

Kisa Bartimayo kutokana na umuhimu wake, kinaandikwa na injili tatu kati ya nne, kilitokea wakati Yesu akiwa katika safari yake kwenda Yelusaremu kusulubiwa na kumkomboa mwanadamu. Bartimayo alikuwa kipofu wa macho na ufahamu wa Yesu pia. Upofu ambao unatukumba hata sisi leo:

Upofu wa mambo ya kiroho:

Upofu wa kutojua nyakati tunazoishi kwamba ni nyakati za hatari, nyakati za mwisho maana mambo yote yaliyotabiriwa yanatimia wala hakuna badiliko lolote katika maisha yetu. Tunakuwa vipofu hatujui hatari kubwa zinazotuzunguka, mwandishi mmoja alisema “tunahatari kubwa sana ikiwa tutapitisha dakika moja bila kuomba.”

Upofu wa ulinzi na uwezeshaji wa Mungu:

Mungu anatulinda na kujali sana mahitaji yetu. Ni upofu tu unaotufanya tusijue msaada wa Mungu aliouweka tayari kwajili Yetu. Gehazi alipata wasiwasi mkubwa baada ya kuona wamezingirwa na majeshi asijue malaika wengi waliokuwa wanawazunguka kuwalinda na kuwapigania kwa sababu ya upofu mpaka mtumishi wa Mungu, Elisha alipoomba afumbuliwe macho.

2 Wafalme 6:17 “Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”

Mara nyingi tunapopata matatizo tunalalamika na kulaani kwa sababu tu ni vipofu hatujui malaika wanaotuzunguka kutulinda.

Biblia inasema, “Malaika wa Bwana huweka kituo wakiwazungukia hao wamchao Mungu na kuwatunza.”

Upofu unaoletwa na dhambi.

Dhambi huleta upofu hasa dhambi zinazotendwa kwa makusudi na zile zisizotubiwa. Ni shetani, mungu wa dunia hii anayewapofusha,

2 Wakorintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”

Upofu wa fursa za maisha.

Mungu ameweka mbele yetu fursa za kutusaidia lakini sababu ya upofu hatuzioni. Hali ya maisha tunayoishi inaweza ikaakisi upofu au uonaji wetu wa fursa za maisha. Fursa katika kilimo, biashara, malezi ya familia, n.k

Mwanzo 21:19 Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Hajiri hakujua uwepo wa maji sehemu aliyopo hadi Mungu alipomfumbua macho na kuiona fursa.

 

2. Jinsi ya kushughulikia hali ya upofu

Kukubali hali ya upofu

Hatari kubwa inayowakumba vipofu ni kujiona kuwa wanaona. Wanasema kauli za kutiana moyo “Mpofuka ukongweni hapotei njia” huku wanasahau kuwa upofu wao unawatenga na nuru ya Mungu bila kujali umri wao katika uzoefu wa kikristo. Hii ndio shida ya kanisa la Laodekia, wanajidhania wanaona kumbe wamepofuka maisha yao yamejaa uvuguvugu na ubinafsi wasitafute msaada wa Mungu ili waone.

Ufunuo wa Yohana 3:17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi..”

Bartimayo alitambua hali yake ya upofu na akawa na shauku ya kuonana na Yesu ili apate uponyaji maana aliisha sikia habari zake. Ni wakati ambapo mdhambi anapoona hitaji la mkombozi, ndipo anapoenda kutafuta msaada wake.

Mtu kama huyo anapoenda kwa Yesu anasema wazi wazi dhambi, makosa, udhaifu au hitaji lake kama vile mtoza ushuru katika mfano wa Yesu kwamba,

Luka 18:13 “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.” Na Mungu atajibu na kutoa msaada.

Kutafuta msaada wa uponyaji

Tatizo kubwa la vipofu ni kutojua nani wa kumwomba msaada. Ni ukweli usiopingika kuwa si kila mtu anaweza kutatua matatizo yetu ya kila siku au kutimiza mahitaji yetu; Hivyo kujua ni mtu wa namna gani wa kumwendea wakati wa hitaji lako ni jambo la mhimu. Mfano mtu akitaka msaada fulani unaohusisha kada fulani ni sharti aende kuuliza katika kada husika vinginevyo hatapata msaada unaotakiwa.

Mungu hutufumbua upofu wetu na nadhani Bartimayo alilitambua hili,

Zaburi 146:8 “Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki”

Bartimayo alijua msaada wake wa uponyaji unapatikana kwa Yesu tu; maana yeye Yesu aliyeyaumba yale macho alijua namna ya kuyapatia nguvu yakaona tena. Tutambue mtu wa kutoa msaada ni hatua ya msingi katika kupata msaada wetu. Luka.18:36-38

36 na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?

37 Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.

38 Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.

Alipiga kelele akiwa na imani kubwa kwamba uponyaji wake upo kwa Yesu ambaye alikuwa anapita.

Kutokata tamaa

Bartimayo hakukata tamaa, alijua hiyo ilikuwa fursa yake ya pekee ya kupata uponyaji wake. ilikuwa fursa ya pekee ya kuweza kuona tena. Watu walipomkataza na kumzuia yeye hakukata tamaa bali alikaza sauti zaidi kuomba msaada wa Yesu.

Luka.18:39 “Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.”

Katika maombi Mungu anatuambia tusikate tamaa.. omba bila kukoma. Wakati mwingine Mungu hatujibu maombi yetu kwa uharaka kama tunavyotaka ili ajue kwamba tunayoyaomba ni hitaji letu hasa au la; na njia ya kuonesha ni hitaji letu hasa nikwa njia ya kuomba bila kukata tamaa.

Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.”

Kutambua hitaji la msingi

Bartimayo alikuwa kando ya njia kila siku akiomba msaada na sadaka kwa watu waliokuwa wanapita njiani ili akidhi mahitaji yake ya kila siku. Huenda upofu wake ulimzuia kuingia katika shughuli za uzalishaji na hivyo akawa ombaomba wa njiani tu. Kama ombaomba wengine hata wa sikuhizi, Bartimayo alikuwa mtu wa kudharauliwa katika jamii.

Jambo linalotia moyo ni kwamba alitambua hitaji lake hasa. Bartimayo hakuhitaji fedha, wala dhahabu au maisha ya ufahari maana alikutana na Yesu ambaye angemtimizia shida yake yoyote. Bartimayo alipoulizwa nikufanyie nini alisema, Luka.18:41-42

41 Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.

42 Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.

Watu wengi huwa tunasahau mahitaji yetu na kukimbilia katika mambo mengine na kupelekea kukosa msaada. Bartimayo hakusema nataka fedha au msaada lakini aliomba apatiwe kuona tena na Yesu akamsaidia.

 

3. Kuwasaidia watu walio katika hali ya upofu

Ni makusudio ya Mungu kwamba tuwasaidie wale walio vipofu wa namna mbalimbali wapate kuona. Ayubu anasema katika maisha yake, Ayubu 29:15 “Nalikuwa macho kwa kipofu, Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea.”

Kazi ya Yesu inatabiriwa na nabii Isaya na Yesu anaidhihirisha kwa huduma yake kuwa ni kuwapatia vipofu kuona tena,

Isaya 42:7 “kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.”

ShareHope Ministry is the independent ministry which aims to proclaim the three angels message of Revelation 14 in the theme of Seventhday Adventist Church. The programs are designed include all people without regarding social, political, econimical and geographical boundaries.